FAHAMU MADHARA YA POMBE KWENYE INI

WATU wengi wanapenda kunywa pombe wakidhani wanajiburudisha lakini ukweli ni kwamba unywaji wa pombe ni hatari kwa afya yako.Watu wanaokunywa pombe hukumbwa na matatizo mengi sana ya kiafya na yale yasiyo ya kiafya, na kundi kubwa zaidi ni la wale wanaolewa kupindukia.Pombe huathiri mifumo yote ya mwili huku ini likiwa katika hatari zaidi kwa vile hilo hufanya kazi ya kuchuja sumu zinazoingia mwilini kupitia mfumo wa chakula, kwa maana hiyo kila sumu iingiayo mwilini lazima ipitie katika ini jambo linalolifanya ini kuwa chombo kilicho katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa mengi zaidi.

Pombe ni kemikali inayopatikana karibu vinywaji vyote vinavyolevya na kitaalamu inaitwa ethanol. Kemikali hii ikiwa katika mwili husababisha matatizo makubwa ya kiafya yakiwamo; kushindwa kufanya kazi kwa ini, uvimbe katika kongosho, saratani na shinikizo la damu.Kwa wanawake wajawaziton unywaji wa pombe ni hatari kwa vile inaweza kukatisha kondo ya uzazi na kumfikia mtoto tumboni jambo linaloweza sababisha kifo cha kichanga hicho.

MADHARA YA POMBE KATIKA INI

Ini hufanya kazi ya kuchuja vyakula na vinywaji tutumiavyo ili kupata virutubisho ambavyo mwili unaweza kuvitumia bila kusababisha hatari ya afya. Pombe pia hupita katika ini na ikiwa katika kiwango kidogo lina uwezo wa kuichakata na isiweze kuleta madhara, lakini katika kiwango kisichoweza vumilika na ini pombe huangamiza seli za ini kwa kiwango kikubwa hivyo kupunguza ufanisi wa kazi zinazofanywa na ini.Kupungua kwa ufanisi wa kazi za ini kunasababu vyakula kutochujwa kwa ufanisi, hivyo baadhi ya sumu huingia moja kwa moja katika mzunguko wa damu na kuathiri sehemu nyingine za mwili.Mwili una kawaida ya kutengeneza seli upya pindi zinapokufa au kuzeeka lakini hili linawezekana tu ikiwa seli zinazotakiwa kutengenezwa zitakuwa katika kiwango ambacho mwili unaweza kumudu.Shambulio la pombe katika seli za ini laweza kuwa kubwa kiasi kwamba mwili unashindwa kumudu kutengeneza seli zinazohitajika, hali hii husababishwa kutengenezwa kwa kovu katika ini.

HOMA YA INI

Kovu katika ini hupunguza uwezo wa ini kunyumbulika na pia kovu ni seli zilizokufa ambazo hazina faida ya kiutendaji mwilini. Uwepo wa seli zilizokufa katika mwili ndio chanzo kikubwa cha saratani.Hali hii ambayo hutokea katika ini hujulikana kama Homa ya Ini ambayo kimsingi husababishwa na virusi aina ya hepatitis lakini aina hii ya homa ya ini huitwa (Alcoholic hepatitis) na huambatana na dalili zifuatazo; Kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika.Dalili nyingine ni maumivu ya tumbo, homa, uchovu wa mwili na kupungua uzito. Homa ya ini inayosababishwa na unywaji wa pombe huweza kuwa ya kawaida au sugu

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*