DIAMOND KIMENUKA TENA :‘KIKUKU’ CHAKE NA USHONGA KWA VIJANA WETU

MIAKA ya nyuma kidogo, mtoto wa kiume akionekana anafanya mambo ambayo yamezoeleka kufanywa na watoto wa kike, wazazi walikuwa wakiumia sana na kufanya jitihada za kumbadilisha. Kwa mfano nakumbuka mmoja wa wadogo zangu alipokuwa mdogo alikuwa akipenda sana kujipikilisha na watoto wa kike. Ninachokumbuka ni kwamba kuna siku mama alimkaripia sana, akamwambia asicheze michezo ya kike. Sikuelewa shida ilikuwa wapi kwa mdogo wangu yule kufanya vile lakini baadaye nilikuja kupata elimu kwamba, mama alikuwa hataki mdogo wangu awe na tabia za kikekike kwani ingekuwa rahisi sana kujiingiza kwenye vitendo vya kishoga.Na kwa nilivyokuwa nikiona tangu zamani, kijana wa kiume ilikuwa ni ngumu kuvaa nguo ambazo zilikuwa zikivaliwa na watoto wa kike, ilikuwa pia si kitu cha kawaida mtoto wa kiume kuvaa hereni, kusuka, kujichubua na vitu kama hivyo lakini leo hii kutokana na kile wanachokiita utandawazi, haya yanafanyika huko mtaani.

Wapo vijana wa kiume ambao ni ‘handsome’, sasa hawa wakiwa wameathirika na utandawazi, wakawa wanasuka, wanavaa hereni, wanajichubua na kujitoboa pua, utapata wakati mgumu sana kusema ni mwanaume, lazima utasema ni mwanamke. Vijana hao wapo wengi sana huko mtaani. Sasa kuonesha kwamba hili ni tatizo kubwa, wapo mastaa wengi sana ambao ndiyo wanaongoza kwenye kujiweka katika mazingira ya kikekike kwa kuiga kutoka kwa wasanii wa nje.Nikisema niitaje orodha hapa inaweza kuwa ndefu lakini kwenye makala haya nataka kumzungumzia staa mkubwa wa muziki hapa Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. Jamaa huyo amepata mafanikio makubwa sana na niseme wazi kwamba, huko mtaani wapo wengi wanaomchukulia kama mtu wao wa mfano ‘role model’. Wanapambana sana wakitamani siku moja wawe kama yeye. Lakini Diamond huyu ndiye anayeongoza kwa kufanya vitendo ambavyo vinaiweka njia panda jamii.

Wakati flani alipokuwa kwenye uhusiano na Wema Sepetu, Diamond aliwahi kuachia picha akiwa amevaa wigi huku akionekana kama aliyerembwa flani hivi. Gumzo kubwa likawa eti anautamani ushoga. Yakasemwa mengi lakini nikagundua alikuwa anatafuta kiki. Watu wamseme weee, kisha yeye aendelee kufanya yake. Hilo kikapita!Baada ya hapo staa huyo akaonekana akiwa amevaa hereni na kuweka kipini puani. Vyote hivyo ni urembo kwa mtoto wa kike. Napo wakasema mengi, mwisho wakanyamaza na hadi leo sehemu nyingi Diamond anaonekana akiwa amevaa hereni, na wakati mwingine anaonekana na kipini puani.

Mimi najua Diamond hajatoboa sikio wala pua bali kipini na hereni anafanya kubandika lakini wengi wanaamini katoboa na hivyo kumuingiza kwenye kundi la wale wenye tabia za kishoga. Yote tisa, kumi juzikati Diamond akiwa kwenye shoo Marekani akaachia picha akiwa amevaa kitu
Picha inayohusiana
mguuni kilichodaiwa ni kikuku. Kitu hicho ambacho hakikuonekana vizuri kwamba kimetengenezwa na ‘matirio’ gani, alikivaa mguu wa kushoto na wafuatiliaji wa mambo ya ‘kishambenga’ wanajua watu wanavyomtafsiri msichana anayevaa kikuku mguu wa kushoto. Kwa kifupi anapewa sifa mbaya.

Sasa licha ya Diamond kuvaa urembo huo juu ya soksi lakini wengi waliishia kusema kavaa kikuku na kuhoji, staa wao huyo anaelekea wapi? Hoja hiyo ndiyo iliyonifanya niandike makala haya. Kwenye ulimwengu wa mastaa kuna kitu kinaitwa kiki na mimi niseme wazi tu kwamba, mambo mengi wanayofanya mastaa ambayo yanaonekana si ya kawaida ni kutafuta kiki tu.Ukifuatilia ishu ya mastaa wa kiume kuvaa hereni na vipini, mastaa wetu wameiga kutoka kwa mastaa wa nje na vile ambavyo tunawajadili kwa kuvaa hivyo, wao wanachukulia poa kwa sababu wanapenda kujadiliwa ili majina yao yawe midomoni kwa watu.

Hata wakati ule Diamond alipopiga picha akiwa amevaa wigi la Wema alijua kabisa atakuwa gumzo. Leo hii kaachia picha akiwa kavaa kikuku, watu wameibua mjadala, yeye yuko zake kimyaa, anapiga pesa zake Marekani huko. Hizo jamani ni staili za kiki tu. Hili la kikuku hata staa wa Marekani, Chris Brown naye juzikati alionekana akiwa amevaa mguu wa kushoto akiwa kwenye shoo.
Tokeo la picha la diamond platnumz zilipendwa image
Kwa maana hiyo basi, tusikimbilie kumpa mtu tabia za kishoga kwa kumuona kavaa hereni, kipini, wigi, kikuku na gauni. Mastaa mara nyingi wanafanya mambo ambayo hayajatarajiwa na wengi ili wazue mjadala, wataongea maneno ya ajabu ili watu waanze kujadili, na katika kujadiliwa huko, majina yao yanazidi kuwa maarufu.

Katika kuhitimisha niseme tu kwamba, asilimia kubwa ya mastaa wanaotikisa duniani wamekuzwa na skendo mbali na kazi zao za kisanii. Leo hii jiulize ni skendo ngapi wamefanya mastaa kama vile Rihanna, Kim Kardashian, Jay Z, Diamond, Wema na wengine unaowajua? Hakika ni nyingi sana! Kwa maana hiyo watu wasidhani eti kwa Diamond kuhusishwa na ushoga kwa kuwa anavaa kikekike inamuuma, wala haimnyimi usingizi kwa kuwa anajua yeye ni mwanaume rijali.Ila sasa ushauri wangu kwa mastaa na hasa Diamond ambaye ni kioo cha jamii ni kwamba, huko mtaani vijana wengi sana wanamuiga kila anachofanya. Kuna vitu anatakiwa kuviacha ili kutokiharibu kizazi chetu. Akiendelea kufanya hayo anayofanya leo kuna siku utashangaa vijana wengi wa kiume huko mtaani wanavaa hereni, wanavaa vikuku, wanajipodoa na kuvyoa viduku wakitaka tu wawe ‘Ki-Diamonddiamond’. Tusifike huko!

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*