FAHAMU TATIZO LA KUTOKWA NA DAMU PUANI

Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtu akatokwa na damu puani, ikiwemo kuumia nje au ndani ya pua, kuwa na shinikizo la juu la damu, matumizi ya muda mrefu ya dawa kama Aspirin, ukosefu wa Vitamin K, unywaji wa pombe uliokithiri au mabadiliko ya homoni hasa kwa wanawake.

Damu inaweza kuwa inatoka kwenye matundu yote ya pua au kwenye tundu moja, inaweza kuwa nyepesi, nzito au inaweza kuwa inatoka kwa mabongemabonge. Inapotokea damu inakutoka puani, lazima ugundue kwamba hicho ni kiashiria kinachoonesha kuwa ndani ya mwili kuna kitu hakipo sawa.

Watu wengi huchukulia tatizo la kutokwa na damu kuwa ni la kawaida, hasa kama damu zitatoka na kukata zenyewe, jambo ambalo ni makosa. Kamanilivyosema, kutokwa kwa damu huashiria kwamba kuna tatizo ndani ya mwili hivyo ni vizuri kuonana na mtaalamu wa afya ambaye atakufanyia vipimo kugundua ni nini kinachosababisha utokwe na damu.

MATIBABU

Simama wima na inamisha kichwa kwa mbele, kusimama itakusaidia kupunguza kasi na msukumo wa damu katika mishipa ya damu puani wakati unapoinamisha kichwa kwa mbele huzuia kumeza damu ambayo italeta shida tumboni. Pia usilale chali maana damu inaweza kurudi na kuziba mirija ya hewa na mgonjwa akashindwa kupumua
Weka pamba au kitambaa chenye uwezo wa kufyonza damu nje ya pua na bana pua kwa muda wa dakika 15 huku ukitumia mdomo kupumua, kubana pua hurudisha damu katika mishipa ya pua na kuzuia kuvuja.
Kuzuia damu isitoke tena usichokonoe pua wala kuinamisha kichwa mbele kwa nguvu na kwa muda mrefu.
Kama damu inaendelea kutoka bana pua kwa kutumia kitambaa chenye ubaridi au barafu
itasaidia kusinyaa kwa mishipa ya damu na kuzuia damu.

Nenda hospitali kama damu puani inatokana na kuumia kichwani, haijakata kwa muda wa dakika 20 na kama pua imeumia au kuvunjika.
ZINGATIA

Kama mtu anatokwa damu puani, lengo lako kubwa la kumsaidia ni kuhakikisha unaondoa au unapunguza tatizo la damu kuendelea kutoka kwa mtu huyu.Wakati unaendelea kumsaidia mgonjwa, inatakiwa uhakikishe anazingatia yafuatayo: Asiongee, ajizuie kukohoa wala asiteme mate. Hii itasaidia kumzuia mgonjwa kuharibu mabongemabonge ya damu ambayo yanaweza kuwa yamejitengeneza puani na kusababisha damu ziendelee kutoka.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*