LULU TENA,MAPYA YAANA KUNIKWATANGU KUTOKA JELA

Siku chache baada ya mrembo Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuachiwa gerezani na kutumikia kifungo cha nje, kikosi cha Operesheni Fichua Maovu cha Global Publisher (OFM) kimemfungia kazi mrembo huyo kwa lengo la kutaka kuona ameyaanzaje maisha hayo mapya ya uraiani.Lulu alibadilishiwa kifungo hicho Jumamosi iliyopita kwa amri ya mahakama ambapo kiu ya mashabiki wa msanii huyo kutaka kujua anaishi wapi ndiyo iliyowasukuma OFM waigie mzigoni.

“Jamani mtujuze basi Lulu anapatikana wapi kwa sasa maana tuna hamu ya kutaka kujua, na je familia yake imempokeaje?” ilikuwa ni simu kutoka kwa msomaji ambaye aliwapigia simu OFM bila kujitambulisha jina. Katika kuanza kufuatilia, awali OFM walinusa habari kuwa msanii huyo anapatikana nyumbani kwao, alipokuwa akiishi na mama yake mzazi Lucrecia Karugila maeneo ya Namanga, Tegeta jijini Dar.

“Lulu tangu ametoka gerezani yupo kwao na tena alivyofika tu amefanyiwa bonge la sherehe,” kilidai chanzo. Baada ya kukusanya data kadhaa, OFM ilifunga safari mpaka nyumbani kwao siku ya Jumanne asubuhi na kukuta hali ya furaha ndani ambapo walipiga hodi kwa muda mrefu bila kufunguliwa.Baada ya kukaa kwa muda wa saa tisa, OFM ilishuhudia Bajaj yenye rangi ya kijani ikifika getini hapo na kupiga honi ambapo ndani ya dakika chache geti lilifunguliwa na mama Lulu akatoka akiwa na mlinzi pamoja na vijana wawili.

Bila kupoteza muda, OFM iliisogelea Bajaj hiyo na kuomba kuzungumza na mama Lulu ikiwezekana kuonana na Lulu lakini bi mkubwa huyo alianza kurusha maneno kwa makachero kama kawaida yake. “Waandishi mmezidi kunifuatilia, kama ni Lulu msubirini mkimpata mtazungumza naye hapa hayupo,” alisema mama Lulu kwa hasira na kupanda Bajaj kisha kuondoka.

Licha ya mama Lulu kusema bintiye hayupo na kumuamuru mlinzi afunge geti kwa funguo kisha kuondoka nao, OFM iliifuatilia Bajaj hiyo hatua kwa hatua ili kujiridhisha kama Bajaj hiyo haikumbeba Lulu.Bajaj hiyo ilielekea katika baa moja iliyopo maeneo hayo na baada ya muda ilifika gari aina ya Toyota Spacio rangi ya bluu bahari na kumchukua mama Lulu huku akimuacha mlinzi na wale vijana kwenye baa hiyo.Baada ya kubaini kwamba Lulu hayupo kwenye Bajaj hiyo, OFM walirudi tena nyumbani kwao na kugonga kwa muda bila majibu ambapo mmoja wa majirani alijitokeza na kudai Lulu amehamishiwa maeneo ya Bahari Beach na wadogo zake.

“Tulimsikia jana usiku na hata leo (Jumatatu iliyopita) akiongea na mama yake humo ndani,” alisema jirani huyo huku akiomba hifadhi ya jina lake.Novemba 13, mwaka jana Lulu aliyekuwa na kesi ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa mpenzi wake, Steven Kanumba, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Hata hivyo, Lulu alihamishiwa kifungo cha nje Jumamosi iliyopita kwa amri ya Mahakama Kuu baada ya kukidhi matakwa ya kisheria.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*